Ujumbe wa Mtendaji Mkuu

Karibu katika tovuti ya Wakala ya Mabasi Yaendayo Haraka (DART) ili upate taarifa zote muhimu kuhusu utekelezaji wa mradi wa DART. Mradi huu ulibuniwa mwaka 2002 na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na kujumuishwa kwenye mfumo wa usafiri wa jiji Aprili 2003 ili kutanzua changamoto za usafiri zilizoathiri wakazi wa jiji la Dar es Salaam na wengine waliowahi kutembelea jiji kwasababu mbalimbali. Miongoni mwa changamoto zilizodumu na kuendelea kudumaza kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya jiji ni pamoja na msongamano wa magari, hali mbaya ya mabasi ya usafirishaji wa binafsi na miundombinuambayo haikuruhusu watumiaji wote wa barabara kufurahia usafiri wao wa kila siku.

Ili kuwezesha mradi kuwa endelevu, Serikali ya Tanzania iliona busara kuanzisha wakala itakayokuwa na mamlaka ya kusimamia mradi huo chini ya Wizara ya Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Katika serikali ya awamu ya tano, mradi wa DART unasimamiwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Kuanzishwa kwa Wakala ya DART tarehe 25 Mei, 2007 kwa mujibu wa Tangazo la Serikali No. 120 ya tarehe Mei, 2007 chini ya Sheria ya Wakala za Serikali No. 30 ya mwaka 1997 uzinduzi wake wa tarehe 16 Juni, 2008 uliandaa mwanzo wa mradi wa DART uliokusudiwa kutekelezwa katika awamu sita. Utekelezaje wa awamu hizo umegawanywa katika makundi mawili ambayo ni uendelezaji wa miundombinu na shughuli za mabasi.

Awamu hizo sita ni:

  • 1)Barabara ya Morogoro, Barabara ya Kawawa Kaskazini, Mtaa wa Msimbazi, na Barabara ya Kivukoni yenye umbali wa kilometa 20.9.
  • 2)Barabara ya Kilwa, Barabara ya Kawawa Kusini yenye umbali wa kilometa 20.3.
  • 3)Mtaa wa Uhuru, Barabara ya Nyerere, Barabara ya Bibi Titi, na Mtaa wa Azikiwe yenye umbali wa kilometa 23.6.
  • 4)Barabara ya Bagamoyo, Barabara ya Sam Nujoma yenye umbali wa kilometa 16.1.
  • 5)Barabara ya Mandela, Barabara Mpya1 yenye ubali wa kilometa 22.8.
  • 6)Barabara ya Mwai Kibaki yenye umbali wa kilometa 27.6.

Awamu ya sita inajumuisha kilometa 130.3.

Utekelezaji wa awamu ya kwanza wa mradi wa DART ulianza Agosti 2010 kwa utengenezaji wa miundombinu ambao ujenzi wake ulikamilika mwaka 2015. Utengenezaji wa miundombinu ya DART umehusisha ujenzi wa barabara, vituo vikuu, na karakana. Vituo Vikuu ni pamoja na Kivukoni kilicho karibu na kivuko cha Kigamboni na soko la samaki, Kimara ambao ni upande wa Magharibi wa njia hiyo, na Kariakoo-Gerezani.

Kituo kingine kikuu ni Morocco kilichoko ncha ya Kaskazini ya Barabara ya Kawawa. Wakati ujenzi wa karakana ya Jangwani umekamilika ujenzi wa karakana ya Ubungo upo kwenye mchakato upo kwenye mchakato.

Kwakuwa ujenzi wa miundombinu wa mfumo wa DART awamu ya kwanza ulikamilika mapema kuliko upatikanaji wa mtoa huduma, serikali iliamua kuanzisha huduma ya mabasi ya muda kwa miaka miwili kama sehemu ya kulinda miundombinu mipya iliyojengwa na fursa ya serikali kupima iwapo mfumowa DART unatekelezeka.

Ili kumwezesha mtoa huduma za usafiri wa ndani kuendesha mfumo wa Mabasi Yaendayo Haraka, serikali imemwomba mtoa huduma wa mabasi wa sasa aunde kampuni itakayoendesha huduma ya mabasi kabla ya mtoa huduma wa kudumu kupatikana.

Tangu tarehe 10 Mei, 2016, Wakala ya Mabasi Yaendayo Haraka ilianza shughuli za mabasi kwa siku tano bila kuwatoza abiria nauli kama sehemu ya kuwazoeza wananchi katika mfumo mpya. Kuanzia Mei 16, 2016 hadi sasa abiria wanalipa nauli nafuu kuanzia shilingi 650 kwa njia kuu na shilingi 400 kwa njia za mlishi. Hivyo, kuna aina mbili za mabasi katika mfumo wa DART, zinazotambulika kama mabasi makubwa ya njia kuu na mabasi madogo ya njia mlishi. Mabasi makubwa ya njia kuu yanabeba hadi abiria 120 wakati mabasi madogo ya njia mlishi yanabeba abiria 50 hadi 60 kwa wakati mmoja.

Maandalizi ya kumpata mkandarasi kwaajili ya uandaaji wa miundombinu ya awamu ya 2 na ya 3 yanaendelea. Kwahiyo, karibu tena katika mfumo wa DART kwa usafiri salama na nafuu.