Habari

Imewekwa: Nov, 14 2018

Jengeni nidhamu ya fedha, acheni vitu vya anasa katika shughuli za ujasiriamali-NEEC

News Images

BARAZA la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) limewataka vijana kuwa na nidhamu ya fedha na uaminifu katika shughuli za ujasiriamali na kuachana na vitu vya anasa ili waweze kukua na kuunga mkono juhudi za serikali za kujenga uchumi wa viwanda hapa nchini.

Hayo yalisemwa na Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Bi. Beng’i Issa wakati akifungua mafunzo ya siku nne ya Program ya Vijana waliohitimu vyuo Vikuu wanaoingia katika ujasiriamali, kuwa wanahitajika kujenga nidhamu ya fedha,uaminifu katika ujasiriamali na kuachana na vitu vya anasa ili waweze kukua na kutoa mchango kwa taifa.

“Baraza tumeandaa mafunzo haya kwa wahitimu wa vyuo vikuu ili kuwapa ujuzi wa kijasiriamali na mkaanzishe au kuendeleza shughuli zenu za ujasiriamali na jiepusheni na vitu vya anasa,” na mafunzo hayo yanalenga maeneo ya utalii, kilimo,nishati mbadala na mazingira, aliongeza kusema, Bi. Issa.

Alisema mafunzo hayo yanawalenga vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 35 kwa kushirikiana na Ubalozi wa Uholanzi lakini awali yalikuwa wanayatoa kwa kushirikiana na wadau wengine katika kuwatayarisha wahitimu wa vyuo vikuu kuwa wajasiriamali.

“Hatutegemei umepata mafanikio kidogo kisha unakimbilia kununua vitu vya anasa, hutafika mbali sababu safari hii siyo ya mteremko”. Hata hiyo aliongeza kusema kuwa mafunzo hayo yameshirikisha vijana 50 ambapo wakike 20 na wakiume 30 na wamewagawa katika madarasa mawili yenye watu 25.

Alieleza kuwa baada ya mafunzo hayo kila mmoja atakuja na wazo la biashara na yatashindanishwa kupata washindi 10 bora na katika washindi hao pia watapata washindi watatu bora ambao wakwanza atapata zawadi mbegu mtaji wa Tsh. milioni kumi, wapili milioni saba na watatu milioni tano.

Bi. Issa alisema juhudi hizo ni katika kuchangia kuelekea uchumi wa viwanda sababu baraza uwezesha viajana kimawazo, maarifa na taarifa na kwa program hiyo ni jambo moja kubwa.

Akitoa mfano alisema vijana wengi waliopata mafunzo kama hayo kwasasa wana kampuni kubwa na wameajiri watu wengi.

Mshiriki wa mafunzo hayo, Bw. Victor Vedasto alisema baada ya kuhitimu alianzisha kiwanda cha kuzalisha unga na chakula cha wanyama kwa kutumia mhogo na hiyo ikamfanya aondokane na tatizo la kubeba bahasha ya kutafuta kazi.

“Kwa sasa wazo langu ni kutumia mhogo na maganda ya viazi kutengeneza wanga ili nizalishe mifuko ya kubebea bidhaa,” hii itasaidia kuondoa tatizo la uchafuzi wa mazingira kutokana na mifuko ya plastiki na pia wanga huo atauza katika viwanda vya nguo na dawa.

Kwa upande wake Dorothea Mukwe alisema yeye ni mbunifu wa kutengeneza picha na mapambo mbalimbali kwa kutumia uzi, misumari na taka mbalimbali.

“Kupitia shughuli hii nimeweza kuajiri watu kusaidia kupunguza tatizo la ajira,” na anasema yeye ni mwalimu wa Halmashauri ya Kisarawe na hivyo anawashauri watumishi wengine kufanya kazi za ujasiriamali baada ya kazi ili kujiongezea kipato.

Naye Meneja Ufuatiliaji na Tathimini wa baraza hilo,Bi. Flora Kajela ambaye pia ni Meneja wa Mradi alisema vijana hao baada ya mafunzo hayo wataunganishwa na wafanya biashara wazoefu ili kupata uzoefu wa kusimamia na kuendesha biashara zao.