Habari

Imewekwa: Apr, 25 2018

Waziri Mkuu apongeza mafanikio ya Baraza

News Images

Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa amevutiwa na mafaniko ya Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi yaliyopatikana katika kipindi cha utekelezaji wa Sera za Serikali ya awamu ya tano.

Aliagiza kuwa ni vema wananchi wakajulishwa mafanikio hayo ili waweze kufahamu jitihada za dhati zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano katika kuboresha uchumi wa wananchi wa Taifa hili.

Waziri mkuu aliyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati baraza hilo lilipokuwa likiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu yake katika kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Januari 2017 mpaka Januari 2018, kuwa baraza liendelee kuelimisha wananchi juu ya mafanikio yaliyopatikana katika uwezeshaji wananchi kiuchumi.

“Nimeyaona mafanikio yaliyopatikana wakati ninapokuwa katika mikoa mbalimbali hivyo ninalitaka baraza kuyaeleza mafanikio haya kwa wananchi,” na nalipongeza Baraza kwa kazi kubwa na nzuri ya kupatikana kwa mafanikio haya, aliongeza kusema,Waziri Mkuu.

Alifafanua kwamba kuna miradi mingi ambayo imewezeshwa katika sekta za kilimo, ufugaji, sekta ya madini hususani wachimbaji wadogo wadogo na uanzishaji wa viwanda vidogo vidogo ambapo yote hayo yanahitaji kuelezewa kwa kina ili wananchi waweze kufahamu.

Pia alisema shughuli za kiuchumi za wananchi pia zimeweza kushiriki katika kuongeza ajira kwa vijana na kulitaka baraza hilo kuendelea kuyatambua makundi ya wananchi hasa vijana na kuyapatia ujuzi ili waweze kujiajiri na kuajiriwa katika sekta mbalimbali.

  1. mkuu Majaliwa aliongeza kusema kuwa serikali imejipanga kuendelea kujenga miundombinu mbalimbali ikiwemo uimarishaji wa nishati ya umeme ili nchini nzima iweze kupata nishati hiyo kwa uhakika ili kuvutia shughuli za uzalishaji mali nchini na kuongeza vipato.

Aidha amelitaka Baraza hilo kujiwekea utaratibu wa kukutana na Ofisi ya Waziri Mkuu mara kwa mara ili kuhakikisha changamoto mbalimbali za kiuwezeshaji zinajadiliwa na kupatiwa ufumbuzi kwa haraka.

Awali, Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Bi Beng’i Issa akiwasilisha taarifa ya uteklezaji wa majukumu ya Baraza hilo, alisema Baraza limefanikiwa kuwezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika uchumi kupitia kushawishi ubadilishaji wa sera na sheria mbalimbali ambazo zinasaidia kuongeza ushiriki wa wananchi kwenye uchumi wa nnchi yao. Katibu Mtendaji huyo pia alieleza kwamba Baraza limekuwa likishirikiana na wadau mbalimbali kufanikisha azma ya kuwezesha wananchi na pia kuwajengea wananchi tabia ya kuweka akiba na kuwekeza katika shughuliza uchumi kupitia vikundi vya kiuchumi.

“Uwezeshaji pia umefanikiwa kutokana na juhudi za Mfuko wa Uwezeshaji Mwananchi wa Baraza kwa kushirikiana na mifuko mingine ya serikali, ambapo mikopo nafuu imekuwa ikitolewa kwa wananchi, kiasi cha takriban watu 1,000,000 wamefikiwa” na hiyo imeleta matokeo makubwa kwa wananchi kushiriki katika uchumi wao, aliongeza kusema,Bi. Issa.

Pia alisema Baraza limejipanga kutekeleza majukumu yake kwa bidii kwa kuhakikisha maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu katika mkutano huo yanafanyiwa kazi kwa kuhakikisha miradi mikubwa ya Serikali inashirikisha vyema watanzania katika ajira na shughuli zingine za kiuchumi na biashara.

Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza hilo, Dkt John Jingu alisema kwamba baraza litaendelea kutilia mkazo katika kuhamasisha wananchi hasa vijana umuhimu wa kujipatia stadi zitazowawezesha kujiajiri na kuajiriwa.

“Hii itaenda sambamba na uhamasishaji, utafutaji na utumiaji wa teknolojia katika kuzalisha mali kuongeza tija na kutafuta masoko,” na msisitizo mkubwa upo katika sekta za kilimo, ufugaji, na uvuvi alifafanua,Dkt. Jingu.

Pia alisema lengo la kufanya hivyo ni kuwezesha nguvu kazi ya vijana takribani 700,000 wanaojiunga na soko la ajira kila mwaka kama chachu ya kupambana vipato duni.